SIASA|MAREKANI
Shirika la Upelelezi la Marekani linachunguza jaribio la mauaji lililomlenga siku ya Jumamosi Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.
Tukio hilo lilifanyika Jumamosi wakati Trump alipokuwa akifanya mkutano wa hadhara katika jimbo la Pennsylvania. Mtu mmoja alifyatua risasi kadhaa na kumjeruhi sikioni Rais huyo wa zamani wa Marekani.
Shirika la upelelezi la Marekani la FBI limesema mwanamume huyo aliyeuwawa mara tu baada ya kufanya shambulio hilo, ametambuliwa kuwa ni kijana Thomas Matthew Crooks mwenye miaka 20 na mkaazi wa jimbo la Pennsylvania. Uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo unaendelea.
Watu walioshuhudia tukio hilo wamesema walimuona mtu mwenye silaha kabla ya shambulio hilo na waliziarifu mamlaka. Hata hivyo polisi wamesema walipokea taarifa kadhaa za shughuli zenye kutia shaka, bila kufafanua zaidi. Mtu mmoja aliyekuwa katika mkutano huo aliuwawa katika shambulio hilo. Rais Joe Biden, amelilaani shambulio hilo dhidi ya Trump na kusema kuwa matukio ya aina hiyo hayana nafasi katika taifa hilo.
Viongozi wa nchi mbalimbali duniani walaani shambulio hilo
Viongozi wa mataifa mbalimbali duniani wamelaani shambulio hilo la risasi lililomjeruhi sikioni aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump. Msemaji wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani na kuliita tukio hilo kuwa ni vurugu za kisiasa.
Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amekitaja kitendo hicho kuwa cha chuki, wakati Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akimtakia Trump nafuu ya haraka. Naye Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema amefedheheshwa na kushtushwa na kilichotokea na ametuma salamu za pole kwa walioathiriwa katika tukio hilo.
Miongoni mwa viongozi wengine waliolaani tukio hilo na kutoa pole kwa Trump ni pamoja na Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg, Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, Fumio Kishida wa Japan, Narendra Modi wa India na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky. soma zaidi