Maofisa wa FBI nchini Marekani wamemtambua mwanaume mwenye umri wa miaka 20 kwa jina la Matthew Crooks kuwa mhusika aliyejaribu kumuua mgombea wa urais kupitia chama cha Republican Donald Trump wakati wa mkutano wa kisiasa huko Pennsylvania.
Taarifa ya FBI kuhusu mhusika aliyejaribu kumuua Donald Trump, imekuja saa chache baada ya tukio la kushtukiza la risasi katika mkutano wa hadhara huko Pennsylvania.
Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump ambaye alipigwa risasi sikioni, yuko katika hali nzuri kwa mujibu wa timu yake ya kampeni.
Rais wa Marekani, Joe Biden amewaoongoza viongozi wengine wa dunia kulaani tukio la mpinzani wake Donald Trump, kushambuliwa kwa bastola akiwa katika mkutano wa kisiasa.
Baadhi ya wanachama wa mrengo wa Trump wametuhumu upande wa Biden kwa tukio hilo.
Viongozi wengine wa dunia akiwemo rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron wamemtakia Donald Trump ahueni ya haraka, Macron ametaja tukio hilo kama pigo kwa demokrasia.
Mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky naye pia ameelani shambulio hilo dhidi ya Trump.
Naye Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya, EU, Ursula von der Leyen ameeleza kushutushwa na shambulio hilo katika mkutano wa kisiasa wa Trump huko Pennsylvania.
Wabunge wa chama cha Republican wameahidi kufanya uchunguzi wa kina katika tukio hilo kubaini namna mtu mwenye silaha alifanikiwa kupita maofisa wenye ulinzi mkali kabla ya kutekeleza shambulio hilo.