Baraza la mawaziri la Israel litakutana kujadili kuidhinishwa kwa usitishaji mapigano ili kumaliza kwa muda uhasama na wanamgambo wa Lebanon Hezbollah.
Makubaliano hayo yatakuwa ya muda wa siku 60 na kujumuisha kuondolewa kwa vikosi vya Israeli kutoka Lebanon, kulingana na ripoti za vyombo vya habari.
Kwa upande wake, Hezbollah ingekomesha uwepo wake kusini mwa Mto Litani, takriban kilomita 30 (maili 18) kaskazini mwa mpaka wa kimataifa, na nafasi yake kuchukuliwa na wanajeshi wa Jeshi la Lebanon.
Hata kama wanadiplomasia walivyopendekeza Jumatatu kuwa makubaliano yamekaribia, mapigano makali yaliendelea, huku mamlaka za Lebanon zikiripoti kuwa takriban watu 31 waliuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel na Hezbollah kurusha makombora kwa Israel.
Mawaziri wanatarajiwa kupiga kura kuhusu mpango huo wakati wa mkutano wa Jumanne, kulingana na Haaretz. Shirika la habari la Reuters lilimnukuu afisa mkuu wa Israel akisema mkutano huo ulinuiwa kuidhinisha maandishi ya makubaliano hayo.
Shirika hilo la habari pia liliripoti vyanzo vinne vyaandamizi vya Lebanon vikisema Marekani na Ufaransa – mshirika wa muda mrefu wa Lebanon – zilitarajiwa kutangaza usitishaji mapigano mara moja.
Kulingana na Idhaa ya 12 ya Israeli, mpango unaowezekana ni pamoja na:
Aidha Marekani itatoa barua ya kutambua haki ya Israel ya kuishambulia Lebanon iwapo Hezbollah itaonekana kukiuka makubaliano hayo.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anasemekana kukubaliana na mpango huo “kimsingi”. Naibu spika wa bunge la Lebanon, Elias Bou Saab, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba sasa “hakuna vizuizi vikubwa” vya kusitisha mapigano “isipokuwa Netanyahu atabadilisha mawazo yake”.
Ofisi ya rais wa Ufaransa ilisema Jumatatu jioni mazungumzo “yamesonga mbele” na kuitaka Israel na Hezbollah “kuchangamkia fursa hii haraka”.
“Tunaamini tumefikia hatua hii ambapo tumekaribia,” msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa la Marekani John Kirby alisema. Lakini aliongeza: “Bado hatujafika.”
Lakini waziri wa usalama wa taifa wa mrengo mkali wa kulia wa Israel, Itamar Ben-Gvir, alizungumza dhidi ya kusitishwa kwa mapigano.
Alisema Israel inapaswa kuendelea na vita hadi “ushindi kamili”, na, akihutubia Netanyahu kwenye X, alisema: “Hatujachelewa sana kusitisha makubaliano haya!”
Mamlaka ya Lebanon imesema makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano yanapaswa kuwekewa mipaka kwa masharti ya azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo lilimaliza vita vya mwaka 2006 kati ya Hezbollah na Israel.
Azimio hilo linajumuisha kuondolewa kwa wapiganaji wa Hezbollah na silaha katika maeneo kati ya Line ya Bluu – mpaka usio rasmi kati ya Lebanon na Israel – na mto Litani, karibu kilomita 30 (maili 18) kutoka mpaka na Israeli.
Israel inasema hilo halikuheshimiwa kikamilifu, huku Lebanon ikisema ukiukaji wa Israel ni pamoja na safari za ndege za kijeshi katika ardhi ya Lebanon.
Ingawa mazungumzo kati ya Israel na Hezbollah yalionekana kuzaa matunda, mazungumzo sambamba ya kumaliza vita huko Gaza yamekwama kwa miezi kadhaa. Mwezi huu, Qatar ilijiondoa katika nafasi yake ya upatanishi kati ya Israel na Hamas, kundi la wanamgambo wa Palestina Israel linalopigana huko Gaza.
Vita nchini Lebanon vilianza tarehe 8 Oktoba mwaka jana wakati Hezbollah iliporusha makombora dhidi ya Israel kuunga mkono shambulio baya la Hamas siku moja kabla.
Lengo la Israel ni kuruhusu kurejea kwa wakaazi wapatao 60,000 ambao wamefurushwa kutoka katika jamii za kaskazini mwa Israel kwa sababu ya mashambulizi ya Hezbollah.
Mwezi Septemba, Israel ilianzisha ongezeko kubwa la vita dhidi ya wanamgambo, na kuharibu miundombinu na silaha zake nyingi, na kumuua kiongozi wake Hassan Nasrallah na viongozi wengine wakuu.
Nchini Lebanon, zaidi ya watu 3,750 wameuawa na takriban 15,600 wamejeruhiwa tangu Oktoba 2023, kulingana na mamlaka ya Lebanon, na zaidi ya milioni moja kulazimishwa kutoka kwa makazi yao.