Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Serikali ya Oman kwa kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo kupitia taasisi mbalimbali za nchi hiyo zinazounga mkono Zanzibar kiufundi na kitaalamu.
Rais Mwinyi amesema hayo Ikulu, Zanzibar, leo Jumatatu Septemba 23, 2024 alipokutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman anayeshughulikia masuala ya Utawala na Fedha, Khalid Almuslahi.
Amesema Serikali Zanzibar itajenga hospitali kubwa ya mkoa katika maeneo ya Mahonda, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambayo itafadhiliwa na Serikali ya Oman.
Rais Mwinyi alimhakikishia naibu waziri huyo uhusiano uliopo baina ya Zanzibar na Oman, ni imara na miradi ya ushirikiano inayoendelea itaendelea kuweka alama muhimu katika kudumisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya pande hizo mbili.
Pia amesema Mji Mkongwe wa Zanzibar, ni eneo muhimu la urithi linalohitaji kuendelezwa wakati wote. Hivyo, juhudi zinazofanywa na Serikali ya Oman za kuukarabati na kuuimarisha ni kuunga mkono jitihada za Serikali za kuinua uchumi wa nchi.
Kwa upande mwingine, Rais Mwinyi amesema mbali na Mji Mkongwe kuwa kivutio cha utalii, pia ni eneo muhimu kwa kukuza uchumi na utamaduni wa Zanzibar, na Serikali itaendelea na juhudi za kuutunza mji huo.