Mlipuko uliosababishwa na uvujaji wa gesi kwenye mgodi wa makaa ya mawe mashariki mwa Iran umeua takriban watu 51, vyombo vya habari vya serikali vilisema Jumapili.
Zaidi ya wengine 20 walijeruhiwa baada ya mlipuko huo katika jimbo la Khorasan Kusini .
Inaripotiwa kusababishwa na mlipuko wa gesi ya methane katika vitalu viwili vya mgodi huko Tabas, kilomita 540 (maili 335) kusini mashariki mwa mji mkuu Tehran.
Mlipuko huo ulitokea saa 21:00 kwa saa za ndani (17:30 GMT) siku ya Jumamosi, vyombo vya habari vya serikali vilisema.
Gavana wa Khorasan Kusini Javad Ghenaatzadeh alisema kulikuwa na wafanyikazi 69 kwenye vitalu wakati wa mlipuko huo.
Kulingana na shirika la habari la AP, alisema: “Kulikuwa na mlipuko na kwa bahati mbaya watu 69 walikuwa wakifanya kazi katika vitalu vya B na C vya mgodi wa Madanjoo .
“Katika kitalu C kulikuwa na watu 22 na katika kitalu B kulikuwa na watu 47.”
Bado haijafahamika ni watu wangapi ambao bado wako hai na wamenaswa ndani ya mgodi.
Vyombo vya habari vya serikali sasa vimerekebisha idadi yake ya awali ya vifo 30.
“Idadi ya wafanyikazi waliokufa iliongezeka hadi 51 na idadi ya waliojeruhiwa iliongezeka hadi 20,” shirika rasmi la habari la IRNA liliripoti.
Ikimnukuu mkuu wa shirika la Hilali Nyekundu la Iran, runinga ya taifa ilisema mapema Jumapili kwamba watu 24 walipotea.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Rais wa Iran Masoud Pezeshkian alitoa rambirambi kwa familia za wahanga.
“Nilizungumza na mawaziri na tutafanya kila tuwezalo kufuatilia,” Pezeshkian alisema katika maoni ya televisheni.
Mgodi wa Tabas unashughulikia eneo la zaidi ya kilomita za mraba 30,000 (karibu maili za mraba 11,600) na una akiba kubwa ya kupikia na makaa ya joto, kulingana na IRNA.
“Linachukuliwa kuwa eneo tajiri na kubwa zaidi la makaa ya mawe nchini Iran,” IRNA ilisema.
Mwendesha mashtaka wa eneo hilo Ali Nesaei alinukuliwa na vyombo vya habari vya serikali akisema “mlundikano wa gesi mgodini” umefanya shughuli za utafutaji kuwa ngumu.
“Kwa sasa, kipaumbele ni kutoa msaada kwa waliojeruhiwa na kuvuta watu kutoka chini ya vifusi,” Nesaei alisema.
Aliongeza kuwa “uzembe na makosa ya mawakala husika yatashughulikiwa” hapo baadaye.
Mwaka jana, mlipuko katika mgodi wa makaa ya mawe katika mji wa kaskazini wa Damghan uliwauwa watu sita, ambayo pia inawezekana ni matokeo ya uvujaji wa methane kulingana na vyombo vya habari vya ndani.
Mnamo Mei 2021, wachimbaji migodi wawili walikufa katika kuporomoka kwa tovuti moja, vyombo vya habari vya ndani viliripoti wakati huo.
Mlipuko wa mwaka 2017 uliua wachimba migodi 43 katika mji wa Azad Shahr kaskazini mwa Iran, na kusababisha hasira dhidi ya mamlaka ya Iran.